MPANGAJI APEWE NOTISI YA MUDA GANI KUONDOKA KWENYE NYUMBA ?.
Kuna matatizo sana kati ya wapangaji na wenye nyumba kuhusu notisi ya kuondoka au kuondolewa. Wako wanaosema notisi ni mwezi mmoja, wako wanaosema ni miezi mitatu n.k. Kama ni kweli ama hapana tutaona hapa sheria inasemaje.
Masuala ya pango yanaongozwa na sheria kuu mbili. Moja sheria ya ardhi namba 4 ya mwaka 1999 na pili sheria ya mikataba sura ya 345. Kwa pamoja sheria hizi mbili husimamia jambo hili.
1.MIKATABA YA PANGO.
Mikataba ya pango inahusisha makubaliano ya upangaji kati ya mwenye nyumba na mpangaji au mpangaji na mpangaji mwingine wa pili. Pango laweza kuwa la nyumba ya kuishi, kwa ajili ya biashara, nyumba ya ibada au shughuli nyinginezo. Yote haya yataingia katika maana ya pango.
2. AINA ZA MIKATABA YA PANGO.
Sheria ya ardhi vifungu vya 78 na 79 inatambua mikataba ya upangaji ya muda mrefu na vipindi vifupi. Inatambua pango la wiki, mwezi, miezi, mwaka na miaka. Imetoa uhuru kwa wahusika wenyewe kuamua ni muda gani wangependa kuingia mkataba.
3. NOTISI YA KUONDOKA.
Katika vitu muhimu sana katika suala la pango ni notisi ya kuondoka au kuondolewa katika pango. Jambo la kuzingatia awali kabisa ni kuwa notisi hii ni muhimu pande zote mbili. Upande wa mwenye nyumba na upande wa mpangaji. Kila mmoja kwa nafasi yake anawajibika kutoa notisi kwa mwenzake panapo mahitaji ya kuondoka au kuondolewa.
Ikumbukwe notisi si kwa ajili tu ya kuondoka na kuondolewa bali pia hutakiwa yanapotokea mabadiliko yoyote katika masharti ya mkataba. Hii ina maana hata kuongeza kodi, kupanga kukagua nyumba, kufanya marekebisho n.k. notisi yafaa itolewe.
4. NOTISI NI YA MUDA GANI.
Sheria haikutamka moja kwa moja notisi ya kuondoka au kuondolewa iwe ya muda gani. Kinachohitajika na cha lazima ni kuhakikisha notisi inatolewa lakini pia inatolewa katika muda unaokadirika na kuingia akilini( reasonable ).
Kwahiyo notisi inaweza kuwa muda wowote isipokuwa muda huo uwe unaokadirika na kuingia akilini.
Ili tujue muda unaokadirika yafaa tuangalie muda wa pango ulio katika mkataba. Kwa mfano mtu mwenye mkataba wa miaka mitano huwezi kumpa notisi ya kuondoka ya mwezi mmoja au hata miwili. Lakini mwenye mkataba wa miezi minne au mitatu unaweza kumpa notisi hata ya mwezi mmoja. Mwenye miezi sita hata miezi miwili inaweza kuwa sawa na wa mwaka miezi mitatu inaweza kuwa sawa.
Jambo moja nisisitize sana hapa. Kwakuwa sheria haijataja wazi muda wa notisi ya kuondoka ni vema sana tena sana kuhakikisha mkataba wenu wa pango unaeleza muda wa notisi. Ni muhimu sana. Mkataba ueleze wazi kabisa notisi itakuwa ni ya muda gani ikiwa mwenye nyumba anataka nyumba yake na ikiwa mpangaji anahitaji kuondoka. Na katika kukubaliana, muda wowote mtakaokubaliana unatosha na unakubalika kisheria kwasababu umetokana na hiari ya mkataba.
Usikubali kusainishwa mkataba ambao hauelezi muda wa notisi . Hili litakuondolea masahibu baadae.
Hapo juu tumesema huwezi kumuondoa mpangaji kwenye nyumba bila kumpa notisi. Hili ni muhimu kulirudia. Notisi ni lazima isipokuwa muda wa notisi ndio utatofautiana.
5. KUMUONDOA MPANGAJI KABLA YA MUDA WA MKATABA KUISHA.
Hili nalo ni kosa na ikitokea basi mwenye nyumba lazima alipe fidia. Hili ni kosa la kuvunja mkataba kama ilivyo kuvunja mikataba katika mikataba mingine yoyote.