YAJUE MAMBO 7 KUTOKA SHERIA YA ARDHI.
Kazi kubwa ya sheria zote zinazoshughulika na masuala ya ardhi ni kuratibu na kutoa mwongozo katika miamala mbalimbali ya masuala ya ardhi katika maisha ya kila siku. Miamala hiyo ni kama uuzaji na ununuzi wa ardhi, masuala ya mikopo na rehani, upangaji na upangishaji, masuala ya fidia, kuhamisha umiliki, haki na wajibu wa mmiliki ardhi, haki na wajibu wa serikali katika ardhi yote, upimaji na ramani, namna ya kutatua migogoro ya ardhi, n.k.
Makala yatagusa kwa mtindo wa dondoo baadhi ya mambo ya msingi yaliyo katika sheria ya ardhi namba 4 ya 1999 sura ya 113.
1.SHERIA NAMBA 4 YA MWAKA 1999.
Sheria hii ilipitishwa na bunge la Jamhuri ya Muungano mwaka 1999. Hata hivyo ilianza kutumika rasmi mwezi mei mwaka 2001.
( a ) MDHAMINI WA ARDHI YOTE NI RAIS.
Sehemu ya pili ya kifungu cha 3 cha sheria hii inaanza kwa kueleza sera ya taifa ya ardhi. Kubwa linalotajwa ni kuwa ardhi yote ni mali ya umma ambayo mdhamini wake ni rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania. Huu ndio msingi mkuu wa ardhi yetu.
( b ) WASIMAMIZI WAKUU WA ARDHI.
Sehemu ya iv kifungu cha 8 mpaka 18 kinaeleza watumishi wakuu na wasimamizi wa ardhi kitaifa. Waziri wa ardhi ndiye mwenye dhamana kuu akifuatiwa na kamishna mkuu wa ardhi kabla ya kutajwa kamishna msaidizi na baadae maafisa ardhi . Wajibu, kazi na majukumu yao yameainishwa katika vifungu hivyo. Sambamba na hilo mipaka katika utekelezaji wa majukumu yao ni jambo jingine lililoainishwa.
( c ) KUMILIKI HATI.
Sehemu ya vi kifungu cha 24 mpaka 30 yameelezwa masuala ya hakimiliki. Taratibu za kupata hakimiliki na umilikishwaji . Wakati huohuo vifungu vya 31 mpaka 35 vimeeleza vyema masharti yanayoambatana na hakimiliki ,muda wa hakimiliki pamoja na kodi za ardhi.
Kifungu cha 76 mpaka 78 kimeongelea uuzaji wa ardhi hasa zenye hati miliki.
( d ) UPANGAJI NA UPANGISHAJI.
Sehemu ya ix kifungu cha 77 mpaka 93 kimeeleza kwa urefu masuala yote ya upangaji katika ardhi. Haki na wajibu wa mpangaji vimeelezwa. Pia aina ya mikataba ya upangaji imeainishwa sambamba na yale mambo ambayo yakifanyika yanaathiri upangaji.
( e ) MASUALA YA MIKOPO .
Sehemu ya x ya sheria hii ni sehemu muhimu sana. Ni sehemu inayoeleza masuala ya mikopo. Imeeleza haki na wajibu wa mkopaji halikadhalika haki za mtoa mkopo. Eneo hili zimejadiliwa rehani pia. Rehani zote yaani zile zitokanazo na hati za kimila kwa ardhi za vijijini na zile zitokanazo na hati zisizo za kimila kwa wenye ardhi mijini.
Haki za mtoa mkopo pale pesa yake inaposhindwa kurejeshwa imeelezwa. Nini afanye,kwa kutumia njia zipi na kwa wakati gani ni sehemu ya maelezo hayo. Wakadhalika hatua anazoweza kuchukua mkopwaji baada ya kushindwa kurejesha .
( f ) HAKI YA NJIA.
Kifungu cha 151 mpaka 156 kimeongelea masuala ya haki ya njia. Hii ni hasa kwa yale maeneo ambayo baadhi ya watu wamejenga kwa kuziba njia. Vifungu vimeeleza haki ya njia kama haki ya msingi katika masuala ya ardhi.
( g ) NGUVU YA MAHAKAMA.
Sehemu ya xiii kifungu cha 187 sambamba na kifungu cha 157 na 158 vimeeleza uwezo na nguvu ya mahakama katika masuala ya ardhi. Mahakama inaweza kutumika mda wowote kwa yoyote anayehisi haki haikutendeka katika ardhi yake. Mahakama ndicho chombo kikuu cha kufafanua sheria hii na kutoa mwongozo kwa pande zinazobishana.